Dodoma — Tanzania imepiga hatua ya kihistoria katika teknolojia kwa kutangaza Sera ya Kitaifa ya Akili Bandia (National AI Policy), ikifanya nchi yetu kuwa moja ya nchi chache za Afrika Kusini mwa Sahara kuwa na mwongozo rasmi wa matumizi ya teknolojia hii inayobadilisha dunia.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye, alisema sera hii itasaidia Tanzania kufaidika na uwezo wa Akili Bandia katika sekta za afya, kilimo, elimu na serikali bila kulazimika kufuata kila kitu kilichoundwa na nchi za nje. "Tunataka AI ya Tanzania kwa wananchi wa Tanzania," alisema Waziri Nnauye.

Sera inazingatia maadili ya matumizi ya AI, ulinzi wa data za kibinafsi, na jinsi ya kuhakikisha kwamba teknolojia hii inawasaidia hasa Watanzania wa vijijini ambao wanaweza kufaidika nazo katika kilimo na afya.